スワヒリ語(Kiswahili)

Wasifu wa Shule ya Sekondari ya Juu ya Keio Shiki

"Keio Gijuku no Mokuteki (Dhamira ya Keio Gijuku)" Yukichi Fukuzawa

Keio Gijuku haitaridhika na kuwa shule ambayo ni kama shule nyengine zinazopatikana kokote. Keio Gijuku ni shule yenye dhamira ya kulea wanafunzi na wahitimu kuwa "chimbuko la hadhi ya utu" na "mfano wa kuigwa wa uwezo wa kufikiri na maadili" nchini Japani. Kimsingi, shule hii inatarajia kwamba wanafunzi wake na wahitimu watakuwa na familia thabiti na kupata kipato chao kwenye jamii, pamoja na kuonyesha wazi umuhimu wa kudumisha uhuru wa taifa na kuwa "viongozi wa jamii," sio tu kwa kulizungumzia hilo, lakini kwa kuchukua hatua wao wenyewe.

 Mwezi Oktoba mwaka 1858, Yukichi Fukuzawa (1835-1901), ambae baadae aliandika makala kadhaa ikiwemo "Gakumon no Susume (Ushawishi wa Kujifunza)" na "Bunmeiron no Gairyaku (Muhtasari wa nadharia ya Ustaarabu") na ambae alikuwa kiongozi wa Japani mpya katika nyanja mbali mbali kama mtu mwenye weledi wa tafakuri, mwana taaluma na mwandishi wa habari, alifungua shule ndogo ya masomo ya Kidachi (baadae ilibadilishwa kuwa shule ya masomo ya Kiingereza) katika eneo la Edo (eneo ilipo Tokyo hivi sasa). Huo ndio mwanzo wa shirikisho la elimu la Keio Gijuku, ambapo taasisi kuu iliyoundwa nayo ni Chuo Kikuu cha Keio, chenye historia ndefu ya kuwa chuo kikuu binafsi kikongwe zaidi nchini Japani. Dhamira iliyowasilishwa hapo juu ya "Keio Gijuku no Mokuteki (Dhamira ya Keio Gijuku)" ni sehemu ya hotuba ya muasisi aliyoitoa mwezi Novemba mwaka 1896 (Meiji 29), na inajuulikana kote kuwa ndio muongozo unaonyesha kwa ufasaha na kwa ufupi malengo ya Keio Gijuku.

Shule ya Sekondari ya Juu ya Keio Shiki ilianzishwa kama shule ya kuendeleza utamaduni wa Keio Gijuku na kama sehemu ya shirikisho hilo katika mji wa Shiki katika Mkoa wa Saitama. Shule hiyo ilikuwa awali Shule ya Sekondari ya Juu ya Kilimo ya Keio, iliyofunguliwa mwezi Mei mwaka 1948. Shule hiyo ilifunguliwa kwenye maeneo ya Chuo Kikuu cha Utabibu na Upandikizaji wa Wanyama ambayo ilihamishiwa kwenye eneo la Shiki kufuatia ardhi na jengo la Taasisi ya Utafiti ya Toho Sangyo kutolewa na Yasuzaemon Matsunaga (1875-1971), ambae ni mhitimu wa Keio Gijuku, kwa Keio Gijuku mwezi Septemba mwaka 1947. Shule ya Sekondari ya Juu ya Kilimo ya Keio baadae iligeuzwa kuwa shule ya sekondari ya masomo yote katika mwezi Aprili mwaka 1957 kwa kubadilishwa jina na kuitwa Shule ya Sekondari ya Juu ya Keio Shiki, jina ambalo linatumika hadi sasa. Ni shule ya wavulana, ambapo takriban wahitimu wake wote huingia katika Chuo Kikuu cha Keio kwa pendokezo la mwalimu mkuu wa shule (takriban wanafunzi 250 kila mwaka).

Leo hii, Shule ya Sekondari ya Juu ya Keio Shiki ina eneo la mita mraba 107,345 na majengo yenye njenzo kamilifu. Ina mandhari mazuri ya asili ikiwemo msitu mzuri wenye masalia ya Musashino. Shule hiyo inatumia vyema mazingira yake yenye wigo mpana na kubuni mitaala maalum ambayo mara nyingi huendelea hadi kiwango cha chuo kikuu cha masomo ya sayansi ya jamii bila ya kujifunga kwenye masomo maalum ya mataarisho ya mitihani ya kuingilia chuo kikuu, wakati huo huo ikiheshimu sifa na upekee wa kila mwanafunzi. Ikiwa na wahitimu wake katika nyanja mbali mbali katika jamii, mpango wa elimu wa Shule ya Sekondari ya Juu ya Keio Shiki unaheshimika kote nchini Japani. Hata hivyo, licha ya kuridhika na mafanikio hayo, wafanyakazi wa Shule ya Sekondari ya Juu ya Keio Shiki wanaendelea kupigania maendeleo zaidi kila siku chini ya miongozo ya malengo na dhamira za elimu, kama hivi ifuatavyo:

Dhamira ya Shule ya Sekondari ya Juu ya Keio Shiki

Dhamira ya Shule ya Sokondari ya Juu ya Keio Shiki ni kutoa elimu ya sekondari ya juu kwa wanafunzi kwenye ngazi ya awali katika matayarisho ya elimu yao katika Chuo Kikuu cha Keio, kwa mujibu wa falsafa ya muasisi wake Yukichi Fukuzawa. Ili kufikia lengo hilo, walimu wetu wamekita juhudi zao katika kutimiza malengo haya manne ya elimu:

1 Kuwafanya wanafunzi kujisikia fahari kuwa sehemu ya shule.
Kulea tabia ya kujitegemea na kujiheshimu na kuwafunza wanafunzi kuwa na ari ya kutenda wao wenyewe, kuwa na taadhima na bashasha.
2 Kuwapa wanafunzi elimu ya msingi.
Kuwafanya wanafunzi waelewe umuhimu wa masomo yao na utafiti na kuwaongoza kushikana na masomo kwa hiari yao ili kuwa na mafanikio kwenye nyanja mbali mbali katika jamii katika siku za usoni, pamoja na kupata elimu ya msingi inayohitajika ili kuweza kusoma katika Chuo Kikuu cha Keio. Hususan, kuweka nadhari kwenye masomo yanayowaongoza yanayoingiliana na masomo ya sayansi jamii ya ngazi ya chuo kikuu na kulenga katika kuimarisha viwango vyao vya kimasomo.
3 Kukuza uwezo na upekee wa mwanafunzi mmoja mmoja.
Kwa kutumia manufaa yatokanayo na wanafunzi ambao sasa wapo kwenye masomo hayo, kutoa elimu mahsusi ambayo itakuza upekee na uwezo wa wanafunzi, huku ikikuza uhusiano wa mwanafunzi mmoja mmoja na walimu.
4 Kuimarisha afya ya wanafunzi.
Bila ya kuweka nadhari kwenye usimamizi wa afya pekee, kumfanya kila mwanafunzi ashiriki kwenye michezo inayowafaa ili kuchukua hatua za kuimarisha afya zao.

Shule ya Sekondari ya Juu ya Keio Shiki ipo dakika 90 kutoka uwanja wa ndege wa Narita, kiasi cha dakika 70 kutoka uwanja wa ndege wa Haneda, takriban dakika 50 kutoka kituo cha treni cha Tokyo na dakika 30 kutoka kituo cha treni cha Ikebukuro. Eneo letu ambalo ni rahisi kufikika linavutia wanafunzi kutoka maeneo mbali mbali ya nchi ikiwemo Mikoa ya Kanagawa na Chiba, pamoja na Tokyo na Saitama. Mbali ya kujishughulisha na masomo, wanafunzi wengi hujishughulisha na shughuli kwenye klabu za wanafunzi, kufanya matamasha mbali mbali kama Tamasha la Mavuno (Tamasha la Shule), na kuonyesha uwezo wa wanafunzi unaokwenda sambamba na falsafa ya "kujitegemea na kujitambua" iliyoanishwa na Yukichi Fukuzawa.
Kwa mujibu wa maelezo hayo yaliyoainishwa, wasifu wa Shule ya Sekondari ya Juu ya Keio Shiki unaweza kuelezewa kwa ufupi, kama ifuatavyo:

Sifa maalum za Shule ya Sekondari ya juu ya Keio Shiki

  • 1.Mtaala maalum wenye wigo mpana
  • 2.Wanafunzi kidogo kwenye madarasa
  • 3.Utamaduni wa Keio Gijuku
  • 4.Ushirika na Chuo Kikuu cha Keio
  • 5.Shughuli mbali mbali nje ya masomo
  • 6.Urafiki thabiti unaopatikana kwenye shule za wavulana pekee
  • 7.Uhusiano na waliohitimu
  • 8.Kujitegemea kwa wanafunzi
  • 9.Eneo kubwa la shule na mandari ya kuvutia
  • 10.Mazingira yaliyotulia kwa masomo na urahisi wa kuyafikia

Historia ya Shule

1858 Yukichi Fukuzawa anaanzisha shule ya masomo ya Kidachi (ambayo baadae inakuwa Keio Gijuku)
1947 Ardhi na majengo ya Taasisi ya Utafiti ya Toho Sangyo yaliyotolewa na Yasuzaemon Matsunaga (1875-1971) yanakuwa sehemu ya Keio Gijuku.
Chuo cha Utabitu na Upandikizaji wa Wanyama kinahamia Shiki
1948 Shule ya Sekondari ya Juu ya Kilimo ya Keio inazinduliwa
1957 Shule ya Sekondari ya Juu ya Kilimo ya Keio inatambuliwa rasmi kama Shule ya Sekonadri ya Juu ya Keio Shiki
1963 Idadi ya wanafunzi wanaopokelewa kwa mwaka wa masomo inawekwa kuwa 250
1968 Jengo jipya la shule (jengo la sasa la shule) linakamilishwa
1972 Sare za shule zinafutwa (sare za majira ya joto pekee, sare za majira ya baridi zianfutwa mwaka 1973)
1988 Chama cha wahitimu wa Keio Shiki kinazinduliwa
1991 Mafunzo ya lugha (lugha 19) baada ya muda wa masomo yanaanzishwa
1996 Sherehe za uzinduzi wa Keio Shiki no Mori (Msitu wa Keio Shiki)
1998 Maadhimisho ya kutimiza miaka 50 ya kuzaliwa
2008 Maadhimisho ya kutimiza miaka 60 ya kuzaliwa, ambayo ni maadhimisho ya miaka 150 ya kuanzishwa kwa Keio Gijuku